MAADILI NA UTAWALA BORA KATIKA BIASHARA: WATAALAMU KUTOKA NCHI MBALIMBALI ZA AFRIKA WAKUTANA TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (wa pili kushoto), akishikana mikono na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili, Ofisi ya Rais, Jaji Mstaafu Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi, wakati wa mkutano wa siku mbili kuhusu Maadili ya Biashara wa Absa BEN-Africa 2026, uliodhaminwa na benki hiyo na kuhitimishwa leo katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa, Mtandao wa BEN-Afrika na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiangazia nafasi ya misingi ya maadili katika kukuza biashara endelevu na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Kutoka kushoto ni Mtaalamu Mwandamizi wa Maadili kutoka Absa Group, Moses Chisadza na Mwenyekiti wa Bodi wa Benki ya Absa Tanzania, Paul Makanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (Katikati), akishikana mikono na Rais wa Mtandao wa Maadili ya Biashara Afrika wa BEN-Africa, Dk. Bryan Robinson, wakati wa mkutano wa siku mbili kuhusu Maadili ya Biashara wa Absa BEN-Africa 2026, uliodhaminwa na benki hiyo, ukihitimishwa leo katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa, Mtandao wa BEN-Afrika na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiangazia nafasi ya misingi ya maadili katika kukuza biashara endelevu na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria na Udhibiti, Alistides Kashasira.

TANZANIA imepata nafasi muhimu katika mijadala ya kimataifa kuhusu maadili ya biashara, uongozi wenye uwajibikaji na utawala bora, baada ya mkutano wa siku mbili wa Absa BEN-Africa 2026 kuhitimishwa kwa mafanikio katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS).

Mkutano huo uliowakutanisha wasomi, viongozi wa sekta binafsi, watunga sera, wasimamizi wa sekta mbalimbali, wanafunzi na wataalamu wa masuala ya maadili kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani, ulijadili nafasi ya misingi ya kimaadili katika kukuza biashara endelevu na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

Mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa Tanzania, Mtandao wa Maadili ya Biashara Afrika (BEN-Africa) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulikuwa na kaulimbiu isemayo “Mitazamo Tofauti kuhusu Maadili ya Biashara: Misingi ya Kiafrika na Zaidi ya Hapo.”

Akizungumza katika hafla ya ufungaji rasmi wa mkutano huo, Dar es Salaam jana, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili, Ofisi ya Rais, Jaji Mstaafu Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi, aliwataka washiriki kutambua kuwa maadili si kikwazo cha maendeleo, bali ni msingi muhimu wa kuyafikia.

Alisisitiza kuwa ustawi endelevu wa kiuchumi, utawala bora na imani ya wananchi kwa taasisi mbalimbali haviwezi kutenganishwa na uongozi unaozingatia maadili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Absa Bank Tanzania, Paul Makanza katika hotuba yake ya ukaribisho, alisisitiza umuhimu wa kuwakutanisha wadau kutoka vyuo vikuu, sekta binafsi, serikali na asasi za kiraia ili kujadili kwa pamoja changamoto na fursa za kimaadili zinazoweza kuathiri mustakabali wa Afrika.

Katika kipindi chote cha siku mbili, washiriki walijadili masuala mbalimbali yakiwemo mitazamo ya Kiafrika na Magharibi kuhusu maadili ya biashara, uhusiano kati ya faida, madaraka na uwajibikaji wa kampuni, ukuaji endelevu wa uchumi, ujasiriamali unaozingatia maadili, uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, maadili katika sekta ya utalii, falsafa ya Ubuntu na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), pamoja na utawala bora katika dunia inayozidi kuunganishwa.

Mijadala hiyo ilihusisha wasomi mashuhuri, viongozi waandamizi wa kampuni, wasimamizi wa sekta na wataalamu wa masuala ya uongozi, ambao walitoa mitazamo na uzoefu wao kuhusu namna ya kuimarisha maadili katika shughuli za biashara na taasisi za umma.

Miongoni mwa hoja muhimu zilizojitokeza ni kwamba Afrika ina falsafa, tamaduni na mifumo yake ya thamani inayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mijadala ya kimataifa kuhusu maadili na uongozi wenye uwajibikaji.

Washiriki walijadili namna falsafa ya Ubuntu, inayosisitiza utu, mshikamano, uwajibikaji wa pamoja na kuthamini maslahi ya wadau wote, inavyoweza kutumika kuimarisha mifumo ya kisasa ya uongozi na uendeshaji wa biashara.

Pia, kulikuwa na mjadala mpana kuhusu uhusiano kati ya kutengeneza faida na kutimiza wajibu kwa jamii, ambapo washiriki walikubaliana kuwa mafanikio ya muda mrefu ya biashara yanahitaji uwiano kati ya malengo ya kibiashara, uwajibikaji wa kijamii, utunzaji wa mazingira na uzingatiaji wa maadili.

Mijadala mingine iligusia umuhimu wa uongozi unaozingatia maadili katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya teknolojia, matumizi ya Akili Unde, mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usawa na matarajio yanayobadilika ya wadau mbalimbali.

Akizungumzia mafanikio ya mkutano huo katika hafla ya ufungaji rasmi wa mkutano huo jijini humo leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser, alisema ubora wa mijadala iliyofanyika katika siku hizo mbili umeonesha kuwa Afrika ina uwezo wa kitaaluma na kiuongozi wa kushiriki kikamilifu katika kuunda mijadala ya kimataifa kuhusu maadili, utawala bora na biashara zinazowajibika.

“Ubora wa mijadala tuliyoishuhudia katika siku hizi mbili umekuwa wa kipekee. Mkutano huu umeonesha kuwa Afrika ina uwezo wa kitaaluma na kiuongozi unaohitajika katika kuongoza mijadala ya kimataifa kuhusu maadili, utawala bora na biashara zinazowajibika."

“Absa tunaendelea kujizatiti kuunga mkono majukwaa yanayoimarisha uongozi unaozingatia maadili, kwa sababu tunaamini kuwa imani, uadilifu na uwajibikaji ni misingi muhimu ya ukuaji endelevu na ustawi wa pamoja,” alisema Laiser.

Kwa upande wa BEN-Africa, waandaaji wa mkutano huo waliipongeza Tanzania kwa kufanikisha tukio hilo na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Absa Bank Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wadau wengine ulikuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo.

Rais wa BEN-Africa, Dk. Bryan Robinson, alisema mkutano huo umeendelea kuthibitisha umuhimu wa kuwa na majukwaa yanayowezesha watu wenye mitazamo tofauti kujadili kwa uwazi changamoto na fursa zinazohusiana na maadili katika maendeleo ya bara la Afrika.

Alisema ushiriki mkubwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo unaonesha kuongezeka kwa umuhimu wa mitazamo ya Kiafrika katika mijadala ya kimataifa kuhusu maadili ya biashara.

Nao uongozi wa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Omari Khalifa Mbura, ulisisitiza umuhimu wa taasisi za elimu ya juu katika kuandaa viongozi wa baadaye wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto tata za kimaadili zinazokabili jamii, biashara na serikali.

Mbali na mijadala rasmi, mkutano huo ulitoa fursa ya kujenga mitandao ya kitaaluma, ushirikiano na kubadilishana maarifa kati ya washiriki kutoka sekta na maeneo mbalimbali.

Baadhi ya washiriki walieleza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya tafiti za kitaaluma, sera za umma na utekelezaji wa shughuli za biashara ili kukuza uongozi wenye maadili katika Afrika.

Kwa ujumla, washiriki walikubaliana kuwa mijadala iliyoanzishwa katika mkutano huo haipaswi kuishia kwenye majadiliano pekee, bali inapaswa kutafsiriwa katika vitendo ndani ya taasisi, kampuni, serikali na jamii mbalimbali barani Afrika.

Mkutano wa Absa BEN-Africa 2026 ulihitimishwa kwa washiriki kujizatiti kuendeleza misingi ya uadilifu, uwajibikaji na uongozi unaozingatia maadili kama nguzo muhimu za maendeleo endelevu na ustawi wa muda mrefu wa Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser akizungumza wakati wa mkutano wa siku mbili kuhusu Maadili ya Biashara wa Absa BEN-Africa 2026, uliodhaminwa na benki hiyo, ukihitimishwa katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), jijini Dar es Salaam, leo. Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa, Mtandao wa BEN-Afrika na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiangazia nafasi ya misingi ya maadili katika kukuza biashara endelevu na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Prof. Omari Mbura akizungumza wakati wa mkutano wa siku mbili kuhusu Maadili ya Biashara wa Absa BEN-Africa 2026, uliodhaminwa na Benki ya Absa, ukihitimishwa leo katika ukumbi wa mikutano wa UDBS, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa, Mtandao wa BEN-Afrika na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiangazia nafasi ya misingi ya maadili katika kukuza biashara endelevu na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (waliokaa Katikati) akipiga picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa benki wakati wa hitimisho la mkutano wa siku mbili kuhusu Maadili ya Biashara wa Absa BEN-Africa 2026, katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), jijini Dar es Salaam, leo.
Share:

PESA ZAKO ZINAKUFANYIA KAZI AU UNAZIFANYIA KAZI?

Fahamu Siri za Usimamizi Bora wa Fedha, Akiba na Ukuaji wa Biashara

Katika maisha ya kila siku, watu wengi hujitahidi kutafuta fedha, kuongeza kipato na kuboresha hali zao za kiuchumi. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, bado wapo wanaojikuta wakipata kipato lakini wakishindwa kufikia malengo yao ya kifedha. Wengine wanafanya kazi kwa miaka mingi bila kuwa na akiba ya kutosha, huku wafanyabiashara wakipata changamoto ya kutenganisha fedha za biashara na matumizi binafsi.

Hali hii inazua swali muhimu: Je, tunafanya kazi kwa ajili ya fedha pekee, au tunajifunza namna ya kuzifanya fedha zetu zitusaidie kufikia malengo tuliyojiwekea?

Ukweli ni kwamba mafanikio ya kifedha hayategemei tu kiasi cha fedha mtu anachopata, bali pia namna anavyopanga, kutumia, kuweka akiba na kuwekeza fedha hizo.

Katika makala hii, tunaangazia misingi muhimu ya usimamizi wa fedha na namna huduma za kibenki zinavyoweza kuwa sehemu ya safari ya mtu binafsi na mfanyabiashara kuelekea maendeleo ya kiuchumi.

Makala hii inawasilishwa kwa mtazamo wa kitaalamu wa Bi. Lilianfavour Makawa, Team Leader – Sales and Service/Support, Benki ya CRDB, Tawi la Ubungo jijini Dar es Salaam.

1. Kipato Kikubwa Si Dhamana ya Mafanikio ya Kifedha

Moja ya dhana ambazo watu wengi wanapaswa kuzitafakari ni kwamba kuwa na kipato kikubwa hakumaanishi moja kwa moja kuwa na mafanikio ya kifedha.

Mtu anaweza kupata mshahara mkubwa lakini mwisho wa mwezi akawa hana fedha za akiba. Vivyo hivyo, mfanyabiashara anaweza kufanya mauzo makubwa lakini akashindwa kuelewa kama biashara yake inapata faida au inaendelea kula mtaji.

Changamoto kubwa mara nyingi huwa katika usimamizi wa fedha.

Kila mtu anahitaji kuwa na mpango wa mapato na matumizi unaomsaidia kujua fedha anazopata zinaelekezwa wapi. Ni muhimu kutambua tofauti kati ya mahitaji ya lazima, matumizi ya kawaida na matumizi yasiyo ya lazima.

Kuweka malengo ya kifedha, kufuatilia matumizi na kuwa na nidhamu ya fedha ni hatua muhimu katika kujenga msingi imara wa uchumi binafsi.

2. Akiba Si Kwa Wenye Pesa Nyingi Pekee

Kuna dhana potofu kwamba kuweka akiba ni jambo linalowezekana kwa watu wenye mishahara mikubwa au wafanyabiashara wanaopata faida kubwa.

Hata hivyo, akiba huanza na utaratibu na nidhamu, si lazima kuanza na kiasi kikubwa cha fedha.

Mtu anaweza kuanza kwa kutenga sehemu ya kipato chake kila anapopokea mshahara au kupata mapato ya biashara. Jambo la msingi ni kuwa na utaratibu unaoeleweka na kuufuata kwa muda mrefu.

Akiba inaweza kumsaidia mtu katika mambo mbalimbali, ikiwemo:

  • Kukabiliana na dharura za kifedha.

  • Kutimiza malengo ya muda mfupi na mrefu.

  • Kupunguza utegemezi wa mikopo kwa matumizi ya kawaida.

  • Kuanzisha au kupanua biashara.

  • Kujiandaa kwa mahitaji muhimu ya baadaye.

Kupitia huduma mbalimbali za kibenki, wateja wanaweza kuchagua njia zinazowasaidia kutunza na kusimamia fedha zao kulingana na mahitaji na malengo yao.

3. Mkopo: Fursa ya Maendeleo au Mzigo wa Kifedha?

Mikopo ni mojawapo ya huduma muhimu zinazoweza kumsaidia mtu binafsi au mfanyabiashara kutekeleza mipango yake ya kifedha.

Kwa mfanyabiashara, mkopo unaweza kuwa fursa ya kuongeza bidhaa, kununua vifaa, kupanua eneo la biashara au kuongeza uwezo wa uzalishaji.

Kwa mtu binafsi, mkopo unaweza kusaidia kutimiza mahitaji maalumu kulingana na masharti ya bidhaa ya mkopo husika.

Hata hivyo, kabla ya kukopa, kuna mambo muhimu ya kuzingatia:

Kwanza, kuwa na sababu inayoeleweka ya kukopa. Usikimbilie kuchukua mkopo kwa sababu tu umeona unapatikana. Jiulize utaufanyia nini na utachangiaje katika kuboresha hali yako ya kifedha.

Pili, elewa gharama za mkopo. Fahamu riba, ada, muda wa marejesho na masharti mengine yanayohusika kabla ya kusaini mkataba.

Tatu, pima uwezo wako wa kurejesha. Hakikisha marejesho yanaendana na kipato chako na majukumu mengine ya kifedha.

Nne, tumia mkopo kwa kusudi lililokusudiwa. Ikiwa umekopa kwa ajili ya biashara, ni muhimu kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika shughuli zinazohusiana na mpango wa biashara.

Mkopo unaopangwa vizuri unaweza kuwa nyenzo ya maendeleo, lakini mkopo usiozingatia uwezo wa marejesho unaweza kuleta changamoto kubwa za kifedha.

4. Benki Si Mahali pa Kuhifadhi Fedha Pekee!

Watu wengi wanapofikiria kuhusu benki, jambo la kwanza linalowajia akilini ni kuweka na kutoa fedha. Lakini huduma za kibenki zina nafasi kubwa zaidi katika maisha ya kiuchumi ya mtu binafsi na biashara.

Benki zinaweza kutoa huduma mbalimbali zinazosaidia katika:

  • Kuhifadhi fedha na kusimamia akaunti.

  • Kurahisisha malipo na miamala.

  • Kuwezesha upatikanaji wa mikopo kulingana na vigezo husika.

  • Kusaidia biashara kusimamia mapato na malipo.

  • Kuwezesha matumizi ya huduma za kidigitali.

  • Kusaidia wateja kupanga na kusimamia mahitaji yao ya kifedha.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa kila mteja kujifunza kuhusu huduma zinazopatikana na kuchagua zile zinazolingana na mahitaji yake.

Uhusiano mzuri kati ya mteja na benki haupaswi kuishia wakati wa kufungua akaunti pekee. Mteja anapaswa kujifunza, kuuliza maswali na kufahamu huduma zinazoweza kumsaidia katika safari yake ya kifedha.

5. Digital Banking: Je, Teknolojia Inarahisisha Maisha Yetu ya Kifedha?

Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa namna watu wanavyofanya miamala na kusimamia fedha zao.

Kupitia huduma za kibenki za kidigitali, wateja wanaweza kupata urahisi wa kufanya miamala mbalimbali bila kutegemea kila wakati kufika katika tawi la benki.

Teknolojia hii ina umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara wanaohitaji kufanya malipo, kupokea fedha na kusimamia shughuli zao kwa haraka.

Hata hivyo, pamoja na urahisi huo, usalama wa taarifa na fedha ni jambo lisilopaswa kupuuzwa.

Kila mtumiaji wa huduma za kidigitali anapaswa:

  • Kutunza siri za PIN na nywila zake.

  • Kutompa mtu mwingine taarifa za siri za akaunti.

  • Kuepuka kubonyeza viungo visivyojulikana vinavyotumwa kwa ujumbe.

  • Kuthibitisha miamala na taarifa za malipo.

  • Kutumia njia rasmi za mawasiliano za benki yake anapohitaji msaada.

Teknolojia inapaswa kuwa nyenzo ya kurahisisha maisha, si chanzo cha kupoteza fedha kutokana na uzembe au udanganyifu.

6. Wafanyabiashara: Tenganisheni Fedha za Biashara na Fedha Binafsi

Changamoto mojawapo inayowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati ni kuchanganya fedha za biashara na matumizi binafsi.

Mfanyabiashara anaweza kufanya mauzo mazuri lakini akashindwa kujua kiasi halisi cha faida kwa sababu fedha zote zinatumika bila utaratibu maalumu.

Ili kuboresha usimamizi wa biashara, ni muhimu:

  • Kutenganisha fedha za biashara na matumizi binafsi.

  • Kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi.

  • Kufuatilia madeni ya wateja na madeni ya biashara.

  • Kujua gharama za uendeshaji.

  • Kutenga fedha kwa ajili ya kukuza biashara.

  • Kutumia huduma za kibenki zinazorahisisha ukusanyaji na usimamizi wa fedha.

Mfanyabiashara anayeelewa mtiririko wa fedha katika biashara yake huwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya maamuzi yenye tija.

Biashara yenye mauzo mengi si lazima iwe na faida kubwa. Muhimu ni kuelewa fedha zinazoingia, zinazotoka na kiasi kinachobaki baada ya gharama zote.

7. Unaanzaje Kujenga Maisha Imara Kifedha?

Mafanikio ya kifedha ni safari inayohitaji mipango, uvumilivu na nidhamu. Hakuna kanuni moja inayofaa kila mtu, lakini kuna hatua ambazo zinaweza kumsaidia mtu kuanza.

Hatua ya kwanza: Jiwekee malengo. Amua unataka kufikia nini kifedha ndani ya miezi sita, mwaka mmoja au miaka mitano.

Hatua ya pili: Tengeneza bajeti. Fahamu mapato yako na panga matumizi yako kabla fedha hazijatumika.

Hatua ya tatu: Jenga utamaduni wa kuweka akiba. Anza na kiasi unachoweza kumudu na ongeza kadiri kipato kinavyoruhusu.

Hatua ya nne: Jifunze kuhusu huduma za kifedha. Usitumie huduma za benki kwa mazoea pekee. Fahamu gharama, faida, masharti na namna zinavyoweza kukusaidia.

Hatua ya tano: Fanya maamuzi kabla ya kukopa au kuwekeza. Chunguza fursa, pima hatari na usifanye maamuzi kwa kushawishiwa na matarajio ya kupata faida ya haraka.

Hatua ya sita: Endelea kujifunza. Maarifa ya kifedha yanakusaidia kufanya maamuzi bora zaidi kadiri mahitaji yako yanavyobadilika.

HITIMISHO: NI WAKATI WA KUIBADILISHA NAMNA TUNAVYOICHUKULIA FEDHA

Kujenga maisha imara kifedha hakumaanishi kuwa lazima uwe na fedha nyingi leo. Kunahitaji kujifunza namna bora ya kutumia kile ulicho nacho, kuweka malengo yanayowezekana na kuchukua hatua zinazokuelekeza kwenye mafanikio ya muda mrefu.

Benki na huduma za kifedha zinaweza kuwa sehemu muhimu ya safari hii, lakini mafanikio yanahitaji pia nidhamu binafsi, maarifa na maamuzi sahihi.

Hatimaye, swali si tu kwamba unapata kiasi gani cha fedha, bali ni nini unafanya na fedha unazopata.

Je, pesa zako zinakufanyia kazi au bado unazifanyia kazi bila mpango wa kuzikuza?


TUSHIRIKISHE MAONI YAKO!

Tungependa kusikia kutoka kwako:

  1. Ni changamoto gani kubwa unayokutana nayo katika kuweka akiba?

  2. Unadhani ni jambo gani muhimu zaidi kabla ya mtu kuchukua mkopo wa benki?

  3. Kama ungepewa nafasi ya kuuliza mtaalamu wa masuala ya kibenki swali moja, ungependa kujua nini?

Andika maoni au swali lako kwenye sehemu ya maoni. Elimu ya fedha inaanza kwa kuuliza, kujifunza na kuchukua hatua.

KUHUSU MTOA MADA

Bi. Lilianfavour Makawa ni Team Leader – Sales and Service/Support katika Benki ya CRDB, Tawi la Ubungo, Dar es Salaam. Kupitia uzoefu wake katika eneo la mauzo na huduma kwa wateja, anawakilisha mtazamo wa kitaalamu kuhusu umuhimu wa huduma za kibenki katika maisha ya watu binafsi na shughuli za biashara.

Makala hii ni kwa madhumuni ya elimu ya fedha na uelewa wa huduma za kibenki. Kwa maelezo kuhusu bidhaa, huduma, gharama na masharti maalumu, wasiliana na benki husika.

Share:

WATEJA CRDB KUFURAHIA MABORESHO YA INTERNET BANKING, KIKOMO CHA MIAMALA KUPANDA HADI SHS MILIONI 200

DAR ES SALAAM; November 5, 2026 - Benki ya CRDB imeboresha huduma yake ya Internet Banking kwa lengo la kuwapa wateja uwezo zaidi wa kufanya miamala, kusimamia fedha zao na kutekeleza mahitaji mbalimbali ya kibenki kwa urahisi, popote walipo.

Maboresho hayo yameangaziwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Internet Banking ni Bora Zaidi – Uwezo Zaidi, Urahisi Zaidi,” inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya kidijitali. Kupitia mfumo huo, wateja wanaweza kupata huduma mbalimbali kwa kutumia simu au kompyuta saa 24 kwa siku, siku saba za wiki.

Kikomo cha miamala chafikia Sh milioni 200

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul, amesema moja ya maboresho makubwa yaliyofanyika ni kuongeza kiwango cha juu cha muamala kutoka Sh milioni 50 hadi Sh milioni 200.
Amesema mfumo huo pia sasa unawezesha wateja kufanya hadi malipo 2,000 kwa muamala mmoja, yakiwamo malipo ya mishahara, jambo linalorahisisha shughuli za biashara na taasisi pamoja na kuokoa muda wa wateja.

Huduma mbalimbali katika mfumo mmoja

Aidha, kupitia Internet Banking, wateja wanaweza kuhamisha fedha kwenda benki nyingine kupitia mfumo wa Tanzania Interbank Settlement System (TISS), kufanya malipo ya kimataifa kupitia mfumo wa SWIFT na kutumia sarafu mbalimbali.
Huduma nyingine zinazopatikana kupitia mfumo huo ni pamoja na malipo ya huduma za Serikali kupitia GePG, kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ununuzi wa umeme wa LUKU, malipo ya ving'amuzi na ununuzi wa tiketi za ndege.

Maboresho hayo yanalenga kuwawezesha wateja kukamilisha mahitaji yao mengi ya kifedha kupitia mfumo mmoja wa kidijitali bila kulazimika kutembelea matawi ya benki.

Usalama wa miamala kupewa kipaumbele

Katika kuhakikisha usalama wa fedha na taarifa za wateja, mfumo wa Internet Banking unatumia njia mbalimbali za uthibitishaji wa mtumiaji, zikiwamo jina la mtumiaji, neno la siri na namba ya uthibitisho ya mara moja (OTP) inayotumwa kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) au kifaa maalumu cha Token.

Hatua hizo zinaongeza ulinzi wakati wa kufanya miamala na kusimamia fedha, kwa wateja binafsi na wa biashara.

Wateja wafurahishwa na maboresho

Baadhi ya wateja waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hiyo wameeleza kufurahishwa na maboresho yaliyofanyika, wakisema yatawasaidia kufanya miamala kwa urahisi zaidi, kuokoa muda na kusimamia shughuli zao za kila siku kwa ufanisi.

Kupitia maboresho hayo, Benki ya CRDB inaendelea kuimarisha huduma zake za kidijitali kwa kuweka msisitizo katika urahisi, ufanisi na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wateja wake.
Share:

DIAMOND TRUST BANK YAZINDUA AKAUNTI YA BIASHARA+ KUIMARISHA UJUMUISHAJI WA KIFEDHA NA KUKUZA BIASHARA NCHINI

Kutoka kushoto: Bw. Abhinav Sharma, Mkuu wa Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi wa DTB; Bi. Elizabeth Mayengoh, Mkuu wa Matawi; Bw. Ravneet Chowdhury, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO); na Bw. Magusa Nhende, Mkuu wa Idara ya Mikopo ya Rejareja na Ubunifu wa Kidijitali, wakati wa uzinduzi wa Akaunti ya Biashara+, huduma iliyoboreshwa inayolenga kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati kupitia huduma za benki zenye gharama nafuu, urahisi wa kufanya miamala na upatikanaji wa huduma za kifedha kidijitali.

Dar es Salaam; November 4, 2026 - Benki ya Diamond Trust Bank Tanzania PLC (DTB) imezindua Akaunti ya Biashara+, huduma mpya ya kibenki inayolenga kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSMEs) kupitia huduma za kifedha zenye gharama nafuu, urahisi wa kufanya miamala na upatikanaji wa huduma za kibenki kidijitali.

Akaunti hiyo imeundwa kwa kutambua mchango mkubwa wa biashara ndogo na za kati katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuchochea ujasiriamali nchini. Kupitia huduma hiyo, DTB inalenga kurahisisha usimamizi wa fedha na miamala ya kila siku ya biashara, huku ikipanua upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha.
Biashara+ inalenga makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, yakiwemo wafanyabiashara wa rejareja, wauzaji na wasambazaji wa bidhaa, wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo, wamiliki binafsi wa biashara pamoja na wajasiriamali wengine wanaohitaji huduma za benki zilizo rahisi na zenye gharama nafuu.

Akaunti Kufunguliwa kwa Shs.10,000

Miongoni mwa vivutio vya Akaunti ya Biashara+ ni urahisi wa kuifungua, ambapo mteja anahitaji kiasi cha kuanzia Sh10,000 pekee, huku salio la chini linalotakiwa kubaki kwenye akaunti likiwa ni Sh10,000.

Hatua hiyo inalenga kupunguza vikwazo vya gharama katika upatikanaji wa huduma rasmi za benki, hususan kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wenye mitaji midogo.
Akizungumza kuhusu uzinduzi wa akaunti hiyo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi wa DTB, Bw. Abhinav Sharma, amesema benki hiyo inaendelea kujizatiti kusaidia ukuaji wa biashara na kupanua ujumuishaji wa kifedha nchini.

"Biashara ndogo na za kati ni mhimili muhimu wa uchumi wetu, na ukuaji wake una mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania. Kupitia Biashara+, tunarahisisha huduma za benki, tunapunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha ili kuwezesha wajasiriamali kutumia muda mwingi zaidi kukuza biashara zao badala ya kuhangaika na miamala ya kila siku," amesema Bw. Sharma.

Manufaa ya Akaunti ya Biashara+

Akaunti ya Biashara+ inakuja na manufaa mbalimbali yanayolenga kurahisisha shughuli za kifedha kwa wafanyabiashara, yakiwemo:
  • Usajili wa bure wa huduma ya Internet Banking.
  • Kujiunga na huduma ya Lipa Eazy bila malipo.
  • Miamala miwili ya bure kwa siku kupitia mfumo wa TIPS.
  • Usajili wa bure wa huduma ya benki kwa simu kwa wamiliki binafsi wa biashara.
Huduma hizo zinawawezesha wateja kufanya na kusimamia miamala ya biashara zao kwa urahisi zaidi, pamoja na kutumia mifumo ya kidijitali katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wa gharama, akaunti hiyo ina ada ya uendeshaji ya Sh2,000 kwa mwezi, huku utoaji wa fedha taslimu kupitia dirishani ukitozwa Sh2,500 kwa kila muamala.

Aidha, miamala ya ziada kupitia mfumo wa TIPS, baada ya kutumia miamala miwili ya bure kwa siku, itatozwa kulingana na viwango vya ada vilivyowekwa na benki.

Masharti ya Kufungua Akaunti

Wateja wanaotaka kufungua Akaunti ya Biashara+ wanatakiwa kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
  • Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au kitambulisho kingine halali.
  • Cheti cha Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
  • Leseni ya biashara, pale inapohitajika.
  • Uthibitisho wa eneo biashara ilipo.
  • Picha ya ukubwa wa pasipoti.
  • Fomu za kufungua akaunti zilizojazwa kikamilifu.
Kwa upande wa kampuni na biashara za ubia, benki inaweza kuhitaji nyaraka za ziada kulingana na aina na muundo wa biashara husika.

Uzinduzi wa Akaunti ya Biashara+ unaashiria hatua nyingine katika juhudi za DTB Tanzania za kupanua ujumuishaji wa kifedha, kuimarisha sekta ya biashara ndogo na za kati na kutoa huduma bunifu za kibenki zinazokidhi mahitaji yanayobadilika ya wafanyabiashara nchini.

Kupitia huduma hiyo, DTB inaendelea kuweka msisitizo katika kuwawezesha wajasiriamali kupata huduma za kifedha zinazowasaidia kusimamia shughuli zao kwa ufanisi na kukuza biashara zao.
Share:

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

Popular Posts

Blog Archive

Labels

Blog Archive

Recent Posts

Label Cloud

BIASHARA (353) BURUDANI (4) KIMATAIFA (10) KITAIFA (132) MICHEZO (41) SIASA (3)

Pages