AIRTEL YASOGEZA SULUHISHO ZA KIDIJITALI KWA WAFANYABIASHARA KATIKA MAONESHO YA TANO YA SIDO KAHAMA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga (wa pili kulia), akikabidhi cheti cha ushiriki kwa Mkurugenzi wa Airtel Tanzania anayesimamia Biashara, Joseph Vipond (kushoto), kufuatia udhamini wa kampuni hiyo katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya SIDO yanayofanyika Kahama, Mkoani Shinyanga. Maonesho hayo yanalenga kukuza biashara na kuhamasisha matumizi ya suluhisho za kidijitali kwa biashara ndogo na za kati (SMEs). Wa nne kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri Salum, akiwa pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Airtel.

Kahama, Shinyanga; Oktoba 24, 2026 - Airtel Tanzania, kupitia kitengo chake cha huduma kwa biashara cha Airtel Business, imewasogezea wafanyabiashara suluhisho za kidijitali na mawasiliano zinazolenga kuboresha ufanisi wa shughuli zao, kupunguza gharama za uendeshaji na kukuza biashara.

Suluhisho hizo zinaangaziwa katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), yanayofanyika katika Viwanja vya Magufuli, Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, kuanzia Oktoba 21 hadi 30, 2026.

Maonesho hayo ya siku 10 yameandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, yakishirikisha zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo 600 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema Serikali inaendelea na juhudi za kupanua upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali ili kuwawezesha kukuza biashara zao, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira.

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za fedha, sekta binafsi na SIDO katika kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wajasiriamali, hususan katika upatikanaji wa mitaji.

“Lengo la Serikali hii ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, hasa wale wenye uwezo wa kuzalisha na kukuza biashara lakini wanaokabiliwa na vikwazo vya kupata fedha za mitaji. Nitumie pia fursa hii kuzihimiza taasisi za fedha kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia SIDO katika kubuni huduma zinazozingatia mahitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuendeleza sekta hii nchini,” alisema Kapinga.

Aidha, Waziri huyo aliiitaka SIDO kuelekeza mikopo zaidi katika shughuli za uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa ili kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza fursa za ajira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Business, Joseph Vipond, alisema ushiriki wa Airtel Tanzania katika maonesho hayo unaonesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuwawezesha wafanyabiashara kupata suluhisho za kidijitali zinazokidhi mahitaji yao na kusaidia ukuaji wa biashara.

“Biashara ndogo na za kati ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania. Ushiriki wetu katika Maonesho ya Kitaifa ya SIDO unaonesha dhamira yetu ya kuwasogezea wafanyabiashara suluhisho za kidijitali zilizo nafuu, za kuaminika na zinazokidhi mahitaji yao."

“Kupitia huduma kama Airtel Chapakazi na SME Bundles, tunasaidia biashara kudhibiti gharama za mawasiliano, kuongeza ufanisi wa shughuli zao na kuzingatia kukuza biashara na kuwahudumia wateja,” alisema Vipond.

Suluhisho za kidijitali zinazolenga kukuza biashara

Katika maonesho hayo, Airtel Business inaangazia suluhisho mbalimbali zilizoundwa kusaidia biashara kuimarisha mawasiliano, kurahisisha malipo na kuboresha upatikanaji wa intaneti.

Airtel Chapakazi

Huduma hii inatoa vifurushi vya data, dakika za maongezi na SMS kwa gharama nafuu, mahsusi kwa wajasiriamali na biashara ndogo na za kati (SMEs). Vifurushi hivyo vinawawezesha wafanyakazi wanaotekeleza majukumu nje ya ofisi kuwasiliana kwa urahisi na wateja pamoja na wenzao.

Airtel SME na Corporate Yatosha

Vifurushi hivi vinatoa suluhisho za mawasiliano kupitia mifumo ya malipo ya baada ya matumizi (postpaid) na mipango mseto (hybrid). Huduma hizo zinajumuisha uwezo wa kugawana vifurushi vya data miongoni mwa watumiaji (data pooling) na mfumo wa mawasiliano ya ndani ya kikundi (Closed User Group – CUG), unaowawezesha wafanyakazi kupigiana simu bila kikomo na bila gharama za ziada kwa mujibu wa masharti ya huduma.

Suluhisho hizi zinalenga kusaidia kampuni kudhibiti gharama za uendeshaji na kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wafanyakazi.

Airtel SmartConnect na Pocket Wi-Fi

Airtel pia inaangazia suluhisho za intaneti kupitia teknolojia za 4G na 5G, zinazosaidia biashara kupata huduma za intaneti ofisini na wanapokuwa safarini. Baadhi ya vifaa vina betri za akiba zinazoweza kusaidia kuendelea kutumia intaneti wakati umeme unapokatika, kutegemea uwezo wa kifaa na upatikanaji wa mtandao.

Airtel Money Enterprise Services

Huduma hii inawezesha biashara kufanya miamala ya kidijitali kwa urahisi na usalama, ikiwemo malipo ya mishahara na ukusanyaji wa malipo kutoka kwa wateja kupitia namba za Till na misimbo ya QR.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya SIDO, Airtel Tanzania inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha wajasiriamali na biashara ndogo na za kati kutumia teknolojia kuboresha shughuli zao.

Suluhisho hizo zinatarajiwa kusaidia wafanyabiashara kuimarisha mawasiliano na wateja, kurahisisha shughuli za kila siku, kuongeza ushindani sokoni na kutumia fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali.
Share:

No comments:

Post a Comment

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

Popular Posts

Blog Archive

Labels

Blog Archive

Recent Posts

Label Cloud

BIASHARA (348) BURUDANI (4) KIMATAIFA (10) KITAIFA (132) MICHEZO (41) SIASA (3)

Pages