15 Januari 2020, Dar
es Salaam. Wateja wa vinywaji vya Sayona,
sasa watakuwa na fahari ya kuchagua zaidi baada ya kampuni inayotengeneza vinywaji
baridi ambayo inakuwa kwa kasi jijini Dar es salaam, Sayona Drinks Limited
kuboresha na kuzindua upya kinywaji kinachofahamika kwa jina la TWIST.
Kampuni ya Sayona
imedhamiria kuwapa machaguo mengi zaidi wateja wake ili kukidhi hitaji za ladha
mbalimbali zinazopendwa na wateja.
Akizungumza wakati wa
hafla ya utambulisho wa bidhaa hiyo, Pawan Patel, Mkurugenzi Mtendaji wa Sayona
Drinks Limited alisema, “Twist ni kiburudisho chenye ladha nzuri, kinachokupa
thamani ya pesa yako. Twist inakuja na ladha saba za kipekee ikiwemo ya
pasheni, chungwa, limao, embe, nanasi, tangawizi na ladha ya Cola,”
Pia amebainisha kuwa
Kampuni itatangaza ujio wa ladha nyingine za kipekee katika siku za usoni.
Aliongeza kuwa, Sayona, imedhamiria kukidhi hitaji la wateja wake ndiyo maana
wameendelea kuwa wabunifu na kila mwaka wamekuwa wakitambulisha bidhaa mpya
sokoni.
“Tunaamini kupitia
Twist, tunayo bidhaa bora ambayo ina utofauti na bidhaa nyingine zilizopo
sokoni, kuwapa wateja wetu kiburudisho chenye ladha nzuri na ya kipekee,"alisema.
Kwa upande wake, Nitin
Menon, Mkurugenzi Mkuu wa Sayona Drinks Ltd Group yeye alizungumzia juu ya
utoaji wao huduma kwa wateja na gharama za bidhaa hii mpya.
Menon alisema, hatua
ya kuizindua Twist ni matokeo ya kazi kubwa inayofanyika ya kuimarisha ukuaji
wa kampuni kupitia mkakati kabambe ambao unaenda sambamba na badiliko la ladha
kwa watumiaji na tabia katika ununuzi.
“Bidhaa yetu mpya ya
Twist inakuja kwa ujazo wa milimita 300 na 400 katika chupa ya plastiki. Bidhaa
itauzwa kwa bei ya rejareja ya shilingi 500 na itapatikana nchi nzima,”
aliongeza.
Aidha, alitumia fursa
hiyo kuutangazia umma kuwa, wameingia makubaliano na staa wa bongo fleva,
Rajabu Abdul Kahali (Harmonize) kuwa balozi wa heshima wa bidhaa za Sayona,
ambaye pia alishiriki katika uzinduzi huo.
“Tunajisika fahari
kuwa na Harmonize kama balozi wa heshima wa bidhaa yetu. Ni miongoni mwa vijana
wapambanaji, mwenye msaada kwa watanzania wengi, anayefanya kazi kwa bidii,
lakini pia amekuwa na chachu ya kuupeleka muziki wa Tanzania mbali zaidi. Hili
ni Jambo ambalo linaunga mkono malengo na maono yetu ya kuwa kinara katika
biashara ya vinywaji baridi barani Afrika,” alisema Menon.
“Tuna imani kwamba
ushirikiano huu utawezesha vinywaji vya Sayona kuwa miongoni mwa bidhaa zenye
nguvu zaidi Tanzania. Harmonize atatusaidia kuwafikia walengwa wetu nchini
Tanzania na sisi kufanya naye kazi kama balozi, ni miongoni mwa hatua muhimu ya
yeye kushiriki katika miradi yetu mingi inayokuja.”
Kwa upande wa
Harmonize, alisema ni jambo la faraja kufanya kazi na Sayona Drinks Limited na
huu ni mwanzo wa ushirikiano mzuri zaidi baina yake na kampuni.
Akizungumzia juu ya
uzinduzi wa bidhaa hiyo, Harmonize amesema, “Twist ni kinywaji kizuri chenye
ladha za kipekee. Nimekuwa nikikitumia mara kwa mara na nimekuwa sehemu ya
ubunifu huu mpya wa bidhaa hii, nina hakika kuwa Watanzania watafurahia bidhaa
hii na matumizi yake yatafika nje ya Tanzania. Pia ninajisikia fahari sana
kujumuishwa ndani ya Sayona Group ambao wamekuwa na sifa kubwa ya ubora wa
bidhaa zao,” alimalizia.
No comments:
Post a Comment