Nukuu sita maarufu za Winnie Mandela


Mwanasiasa na mwanaharakati aliyepigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini Winnie Madikizela-Mandela alifariki dunia Jumatatu akiwa na miaka 81.

Alikuwa mke wa zamani wa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini Nelson Mandela lakini alikuwa na msimamo mkali zaidi kumshinda hata Bw Mandela mwenyewe.

Winnie alifahamika sana na wengi kama Mama wa Taifa.

Alikuwa nembo kuu ya vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, na ingawa sifa zake ziliingia doa miaka ya baadaye, lakini bado alitambuliwa kama mtetezi wa wanyonge.

Alisalia kuwa mwanachama wa chama tawala cha African National Congress (ANC) ingawa nyakati za karibuni alikuwa akikosoa uongozi wa chama hicho
.
Hapa, tunaangazia nukuu sita maarufu ambazo alwiahi kuzitoa.

Kuhusu kufungwa gerezani:


"Miaka niliyofungwa gerezani ilinifanya kuwa mkakamavu... Huwa sina tena hisia za woga ... Hakuna chochote ambacho naweza kukiogopa. Hakuna kitu ambacho sijatendewa na serikali. Hakuna uchungu ambao zijakumbana nao."

Nukuu hii katika kitabu chake cha Lives of Courage: Women for a New South Africa(Maisha ya Ujasiri: Wanawake wa Afrika Kusini Mpya), inaashiria jinsi Bi Madikizela-Mandela alivyofanyiwa ukatili na serikali ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Alifungwa jela mara nyingi kuanzia 1969 na muda mwingi alikuwa amefungwa bila kuwa na ruhusa ya kukutana na wafungwa wengine.

Mwaka 1976, mwaka wa maandamano ya Soweto, alifukuzwa kutoka mji wake na kulazimishwa kuishi maeneo ya mashambani.

Wakati mmoja nyumba yake ilichomwa moto.

Bi Madikizela-Mandela alikuwa mwanasiasa kivyake, na alipinga hatua ya mumewe ya kushauriana na watawala wa ubaguzi wa rangi.

Alidai hilo lingesababisha "usaliti" wa watu weusi.

Licha ya tofauti zao, Bi Mandela alimteua kuwa waziri msaidizi serikali yake ya kwanza 1994.

Alimfuta kazi mwaka mmoja baadaye, lakini Bi Mandela alipinga hilo mahakamani na kufanikiwa. Lakini alifutwa kazi tena.

Jinsi watu weusi watapata uhuru:


"Kwa viberiti vyetu na mikufu yetu tutaikomboa nchi hii."

Tamko hilo, katika mkutano wa siasa mjini Johannesburg, aliashiria kwamba Bi Mandikizela-Mandela alikuwa ameidhinisha na kuunga mkono njia katili ya "kuweka mikufu" - njia ya kuweka matairi shingoni washukiwa wa usaliti na kuwachoma moto wakiwa hai.

Hilo lilishangaza dunia na kutia doa sifa za ANC. Tamko hilo lilishutumiwa na wengi, akiwemo mshindi wa tuzo ya Nobel Askofu Mkuu Desmond Tutu (pichani juu).

Kuhusu kumpenda Nelson Mandela:


"Nilikuwa na wakati mdogo sana kumpenda. Na upendo huo umedumu miaka hii yote ambayo tulitenganishwa... pengine kama ningepewa muda wa kutosha wa kumfahamu vyema zaidi pengine ningegundua kasoro nyingi, lakini nilikuwa tu na wakati wa kumpenda na kumkosa sana wakati wote."

Nelson na Winnie Mandela walikuwa wanandoa waliokuwa maarufu zaidi Afrika Kusini.

Alitambuliwa na wengi kama "mama wa taifa" na aliweka hai jina la mumewe miaka 27 aliyokuwa gerezani.

Alikuwa mfanyakazi wa kutoa huduma kwa jamii alipoolewa na Bw Mandela ambaye tayari alikuwa mmoja wa viongozi wa ANC mwaka 1958. Bw Mandela alihukumiwa jela maisha mwaka 1961 kwa mchango wake katika kupigana na utawala wa makaburu.

Kuhusu kusalia na jina la Mandela baada ya talaka:


"Mimi ni mazao ya wananchi wa taifa hili. Mimi ni mazao ya adui wangu mkuu."

Wawili hao walitalikiana mwaka 1996, miaka miwili baada ya Bw Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini. Miaka ambayo walikaa bila kuonana yamkini iliathiri uhusiano wao. Bi Madikizela-Mandela alituhumiwa kuwa na uhusiano nje ya ndoa.

Alidumisha jina la mumewe wa kwanza jambo ambalo wakosoaji walilitazama kama mpango wake wa kuendelea kufaidi kutokana na nembo ya Mandela.

Kuhusu wanawake:


"Wengi wa wanawake huupokea mfumo dume bila kuuliza maswali na hata huutetea, kwa kuelekeza mahangaiko yao sio kwa wanaume bali dhidi yao wenyewe wakishindania wanaume walio wana wao wa kiume, wapenzi wao na waume zao. Kitamaduni, mke ambaye amedhalilishwa hujituliza na kuelekeza ghadhabu zake kwa wakwe. Kwa hivyo, wanaume huishia kuwatawala wanawake kupitia juhudi za wanawake wenyewe."

Bi Madikizela-Mandela alisifiwa na wafuasi wake kama mtetezi wa haki za wanawake.

Alikuwa kiongozi wa vuguvugu la wanawake katika ANC baada ya chama hicho kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake tena mwaka 1990.

Aliamini kwamba wanawake weusi walitatizwa na nira aina tatu za ukandamizaji - jinsia yao, rangi na tabaka.

Kuhusu serikali ya ANC:


"Ninaamini kuna kitu ambacho ni kibaya sana katika historia ya taifa letu, na jinsi ambavyo tumeiharibu African National Congress."

Katika miaka yake ya baadaye, Bi Madikizela-Mandela alivunjwa moyo na ANC - chama cha zamani cha ukombozi ambayo kiliingia madarakani mwaka 1994 - hii ni kwa sababu ya ufisadi na unga'ng'aniaji wa mamlaka miongoni mwa viongozi wake.

Aliendelea kukiunga mkono lakini alionekana kumuunga mkono Cyril Ramaphosa alipochukua uongozi kutoka kwa Jacob Zuma mapema mwezi huu.
Share:

No comments:

Post a Comment

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

Popular Posts

Blog Archive

Labels

Blog Archive

Recent Posts

Label Cloud

BIASHARA (255) BURUDANI (4) KIMATAIFA (10) KITAIFA (114) MICHEZO (38) SIASA (3)

Pages