BENKI YA ABSA TANZANIA YATHIBITISHA UPYA DHAMIRA YAKE KUKUZA VIPAJI VYA NDANI NCHINI TANZANIA

 

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Patrick Foya (wa tano kushoto), akipokea tuzo ya shukrani ya udhamini kutoka kwa Mwanzilishi wa Jukwaa la Fanisi, Bi. Sarah Majengo, wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Fanisi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Pichani (wa tatu kulia) ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi (TISEZA), Bw. Gilead Teri, pamoja na wafanyakazi kutoka Absa.

Benki ya Absa Tanzania imethibitisha upya dhamira yake ya kukuza vipaji vya ndani na kuimarisha maendeleo ya nafasi za uongozi nchini Tanzania kupitia ushirikiano wake na jukwaa la Fanisi.

Akizungumza wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Jukwaa la Fanisi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Patrick Foya, alisema benki hiyo inajivunia kushirikiana na mpango unaoendelea kulea kizazi kipya cha viongozi nchini.

Akihutubia wageni, washirika, wahitimu na washiriki wa jukwaa hilo, Bw. Foya alisifu maono ya mwanzilishi wa Fanisi, Bi. Sarah Majengo, na kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jukwaa hilo limewabadilisha wataalamu wa ngazi ya kati kuwa viongozi imara wa mashirika kwa kuziba mapengo ya vipaji na kufafanua upya uongozi wa kisasa katika ukanda huu.

Alibainisha kuwa ushirikiano wa Absa na Fanisi unalingana na dhamira ya benki ya kuimarisha mustakabali wa Afrika kupitia uwekezaji kwa watu na maendeleo ya uongozi.

Katika Absa, dhamira yetu ni ‘kuimarisha Afrika ya Kesho, Pamoja, Hatua moja baada ya Nyingine’, na kwetu yote huanzia kwa watu wetu,” alisema. “Tunakusudia kujenga viongozi kutoka ndani. Tunaita kukuza idadi yetu wenyewe, ikimaanisha kuwekeza kwa watu wetu na kuwasaidia kukua kuwa viongozi imara.”

Bw. Foya alitanabaisha kuwa tangu kuanza kushirikiana na Fanisi mwaka 2024, benki hiyo tayari imeona takribani wafanyakazi 40 wakihitimu kupitia jukwaa hilo, huku wengine 28 wakiwa wamejiunga katika awamu mpya.

Kama wadhamini, uamuzi wetu wa kuwekeza katika Fanisi ulikuwa rahisi; tunaamini kuwa kuimarisha vipaji vya ndani ndiyo njia bora zaidi ya kuendesha ukuaji endelevu wa uchumi,” alisema.

Awali, Mwanzilishi wa Jukwaa la Fanisi, Bi. Sarah Majengo alisema jukwaa hilo la kujifunza lilianzishwa ili kuziba pengo kati ya malengo ya kitaifa ya Tanzania na mahitaji ya maendeleo ya rasilimali watu nchini.

Alisema kuwa biashara ndogo na za kati (SMEs) zinachangia zaidi ya asilimia 90 ya biashara nchini Tanzania, zinawaajiri zaidi ya watu milioni tano na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa (GDP).

Hata hivyo, biashara nyingi bado zinakabiliwa na changamoto ya kupata wataalamu wenye nidhamu na uwezo licha ya kuongezeka kwa kiwango cha elimu. Utafiti wa Benki ya Dunia unasema vyeti vya kitaaluma pekee havichukuliwi tena kama viashiria vya kuaminika vya uwezo, huku kampuni nyingi zikihangaika kupata wafanyakazi wenye ujuzi na uwezo,” alisema.

Akihusisha suala hilo na matarajio makubwa ya maendeleo ya Tanzania chini ya mpango wa Taifa wa Vision 2050, unaolenga kujenga uchumi wa trilioni moja unaoendeshwa na tija na ubunifu, Bi. Sarah alibainisha kuwa mijadala mingi kuhusu Vision 2050 inalenga iwapo Tanzania inaweza kukuza watu wake kwa haraka vya kutosha ili kudumisha matarajio hayo. Alisisitiza kuwa pengo kati ya matarajio ya Tanzania na rasilimali watu wake ndilo hasa pengo ambalo Fanisi ipo kulishughulikia.

Alisema kuwa Fanisi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeendesha programu zinazowanufaisha vijana na watu wazima, huku ikiendelea kuboresha dhamira yake kama kichocheo cha maendeleo ya watu.

Kwa upande wetu Fanisi, tumejizatiti zaidi kuhakikisha watu wengi wanapata nafasi ya kufikia uwezo wao kamili,” aliongeza.

Fanisi ni jukwaa la kujifunza na mshirika aliyewekeza katika kukuza vipaji kwa makampuni na watu wenye malengo ya ukuaji, ikitoa mafunzo maalum, fursa za mtandao na uwekaji wa kimkakati.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Patrick Foya (kushoto), akihutubia washiriki wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Jukwaa la Fanisi, zilizodhaminiwa na benki hiyo, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Patrick Foya (kulia), akibadilishana mawazo na washiriki wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Jukwaa la Fanisi, zilizodhaminiwa na benki hiyo, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Patrick Foya (kushoto), akisalimiana na washiriki wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Fanisi Platform, zilizodhaminiwa na Absa Bank, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Katikati ni Bw. Christopher Shayo na Bw. Rwebu Mutahaba.
Mwanzilishi wa Jukwaa la Fanisi, Bi. Sarah Majengo (kushoto), akihutubia washiriki wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya jukwaa hilo, zilizodhaminiwa na Benki ya Absa, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi (TISEZA), Bw. Gilead Teri (katikati), pamoja na Mwanzilishi wa Jukwaa la Fanisi, Bi. Sarah Majengo (kulia kwake), wakipiga picha ya kumbukumbu na washirika, wahitimu na wadau wa jukwaa hilo wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya Fanisi Platform, zilizodhaminiwa na Benki ya Absa, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Share:

No comments:

Post a Comment

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

LILIAN-FAVOUR MAKAWA

Popular Posts

Blog Archive

Labels

Blog Archive

Recent Posts

Label Cloud

BIASHARA (321) BURUDANI (4) KIMATAIFA (10) KITAIFA (123) MICHEZO (41) SIASA (3)

Pages