BENKI ya TPB imepata faida ya Shilingi bilioni 21 kabla ya kodi kwa mwaka 2020. Kiasi hicho ambacho kimepatikani kabla ya kodi, kinatajwa na uongozi wa benki kuwa ni kikubwa ukizingatia changamoto mbalimbali zilizojitokeza mwaka jana, hasa janga la Corona lililoathiri dunia nzima.
Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa wanahisa jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi wa benki hiyo, Dkt. Edmund B. Mndolwa alisema benki hiyo inaendelea kufanya vizuri kwa kupata faida hiyo kabla ya kodi.
Utendaji kazi uliotukuka, ufanisi na umakini wa menejimeti ya benki huku wakisimamiwa kwa karibu na Bodi tumeweza kupata faida kubwa ambalo ni jambo la kujivunia sana kwa kufanya kazi kubwa kwa tija,’’ alisema Dkt. Mndolwa.
Alisema kwamba pamoja na kwamba benki hiyo ina mtaji mdogo, ikilinganishwa na benki nyingine, imeendelea kufanya vizuri katika nyanja zote kwa miaka takriban kumi.
Dkt. Mndolwa alisema kwamba benki hiyo itaendelea kujipanga na kupanua shughuli zake za kibenki nchini na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi kwa sasa katika sekta ya fedha nchini.
Benki ya TPB ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 11 ya mwaka 1991, kama ilivyofanyiwa mabadiliko mwaka 1992. Mwaka 2016 jina la Benki lilibadilishwa na kuwa Benki ya TPB badala ya Benki ya Posta Tanzania.
Katika kuendelea kuelezea matukio makubwa Kwa mwaka 2020, Dkt. Mndolwa alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliziunganisha Benki ya TPB na Benki ya Biashara ya TIB.
Lengo likiwa kuunda benki kubwa ya serikali itakayo boresha huduma, kupanua wigo wa mtandao na kutengeneza faida kubwa.
Benki ya TPB itaendelea kuboresha huduma zake na kubuni huduma mpya zinazokidhi matarajio ya wateja na kuwafikia wateja wengi zaidi wa kipato cha chini. Miongoni mwa huduma kama hizo ni SONGESHA na M-KOBA ambazo zinatolewa na Benki ya TPB kwa kushirikiana na Kampuni ya simu ya Vodacom.
Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Edmund Mndolwa akimalizia taarifa yake amesema Benki ya TPB inafanya vizuri katika soko la mabenki na hivyo kutoa wito kwa wateja kuendelea kuiunga mkono Benki yao. Mwelekeo ni mzuri na ndiyo maana benki imeendelea kukua na hadi kufikisha thamani ya Mali za Shilingi trioni moja mwisho mwa mwaka 2020 ikishika nafasi ya Saba kati ya benki zaidi ya 50 kote nchini.
No comments:
Post a Comment