SHULE YA SEKONDARI YA WAVULANA - SULLIVAN PROVOST
SIKU YA KUTOA ZAWADI KWA WAHITAJI
22 - JUNI KILA MWAKA
Historia
Desemba mwaka 2019, Meneja wa shule, Mhandisi, Marehemu Eric Samwel Mkami alipendekeza shule ianzishe siku ya kutembelea vituo vya kulelea watoto (au watu wazima) wanaoishi kwenye mazingira magumu, kutembelea hospitali moja au Magereza na kuwapa zawadi mbalimbali. Wazo hili lilikuwa na lengo la kujenga utamaduni wa utoaji kwa wanafunzi wetu lakini zaidi kujenga utamaduni wa kumshukuru Mungu kwa kuwapa neema ya kuwa na wazazi au walezi wanaowahudumia vizuri na kuwapatia elimu bora kwa kuwapeleka shule bora ya Sullivan. 2Korintho 9:6-9
Zawadi hizi zitakusanywa toka kwa wanafunzi na wadau wengine wenye mapenzi mema na shule yetu ya Sullivan Provost mara moja kila mwaka. Zawadi hizi zitajumuisha, Nguo, Viatu, madaftari, kalamu, Vyakula na vinginevyo vyenye thamani kama vifaa vya michezo, sabuni, mafuta ya kujipaka, dawa za meno, miswaki n.k. Hii ni nafasi ya pekee kwa shule yetu kurudisha shukrani kwa Muumba wetu kwa mambo mengi makubwa anayotutendea (Zab 116:12)
Kwanini Tarehe 22/06 kila Mwaka?
Hii ni kutimiza ndoto alizokuwa nazo Meneja wetu wa shule, Mtoto wetu na Rafiki yetu, Mhandisi Eric Samwel Mkami aliyefariki tarehe 22/06/2020 na kuacha hili zoezi liendelee kukamilishwa akiwa pamoja nasisi Kiroho.
Ni nani wanahusika kutimiza ndoto hii?
Wadau wote wenye mapenzi mema na Shule ya Wavulana ya Sullivan Provost: Ndugu na Marafiki wa Marehemu Eric Samwel Mkami, Waalimu, Wanafunzi, Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wanaosoma na wanaotarajia kuwaleta watoto wao katika shule yetu, Majirani na yeyote atakayeguswa na huduma hii.
Ufikishaji wa Taarifa kuhusu Siku ya Kutoa Zawadi kwa Wahitaji: Matangazo yatatolewa katika Radio/TV, Barua kwa wadau, Mitandao ya kijamii na taarifa toka kwa mtu kwenda kwa mtu mwingine.
Uzinduzi Rasmi wa Utamaduni wa Siku ya Kutoa Zawadi Kwa Wahitaji.
Uzinduzi utafanyika tarehe 22/06/2021 siku ambayo Marehemu Eric Samwel Mkami atatimiza Mwaka Mmoja tangu kufariki kwake. Siku hiyo tutatoa Zawadi ya Nguo za Marehemu pamoja na Zawadi zingine zitakazo kusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali kama ilivyoainishwa hapo juu. Uzinduzi huu utafanyika katika kituo kiitwacho ‘Child in the Sun’ kilichoko Mbezi Makabe kinachowalea watoto wa kiume waliotoka katika mazingira magumu. Kituo hiki kiko chini ya Mwamvuli wa Kanisa la ‘Roman Catholic’.
Nani Watakaowakilisha Zawadi hizi? – Wawakilishi toka Familiya ya Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Sullivan Provost yaani Wanafunzi, Waalimu, Marafiki, na wadau wengine watakao pata nafasi ya kuhudhuria kwenye tendo hili.
Yesu Mwenyewe alisema: “…Ni heri kutoa kuliko kupokea” Matendo 20:35
Kwa Mawasiliano: 0715210812/0754210812
No comments:
Post a Comment