Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya NBC, Nd Raymond Urassa akizungumza na viongozi wa vyama zaidi ya 200 vya ushirika (AMCOS) Mkoani Tabora wakati wa kongamano lilioandaliwa na benki hiyo lenye lengo la kuwapa mafunzo mbalimbali yakiwemo umuhimu wa huduma za bima, matumizi ya fedha za kigeni pamoja na elimu ya kuweka kumbukumbu za hesabu na matumizi sahihi ya mapato yao ili waweze kukopesheka kwa urahisi. Hafla hiyoimefanyika mkoani humo jana
Benki ya NBC kupitia huduma yake ya #NBCShambani inayowalenga wateja wanaojishughulisha na kilimo imeongoza semina ya mafunzo kwa viongozi wa vyama zaidi ya 200 vya ushirika (AMCOS) Mkoani Tabora kwa lengo la kuwapa mafunzo mbalimbali yakiwemo umuhimu wa huduma za bima, matumizi ya fedha za kigeni pamoja na elimu ya kuweka kumbukumbu za hesabu na matumizi sahihi ya mapato yao ili waweze kukopesheka kwa urahisi. Hafla hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tabora, Nd Bosco Ndunguru na kuhudhuriwa na wadau mbali mbali akiwemo Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Nd Absalom Cheliga na wakulima wa zao la tumbaku kutoka wilaya za Tabora Mjini, Sikonge na Uyui.
Pamoja na kuendesha mafunzo hayo Benki ya NBC kupitia Meneja wa Wateja Wadogo, Nd Raymond Urassa walitoa zawadi ya pikipiki kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Solelansabo, Bi Mary James Merrick ili kumsaidia katika shughuli za kuendesha chama na kuwatembelea wakulima. Pamoja na zawadi ya pikipiki hiyo, Benki ya NBC pia ilitoa baiskeli tatu kwa wakulima kutoka kwa vyama vya msingi mbali mbali kama pongezi kwa juhudi za kupata mazao mengikwa msimu uliopita.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mkurugenzi wa Manispaa ya hiyo, Nd Bosco Ndunguru aliipongeza Benki ya NBC kwa kuwawezesha na kuwapa mikopo na huduma za kibenki zenye gharama nafuu wakulima wa zao la tumbaku ambalo kwa kiasi kikubwa linalochangia pato la mkoa huo. Aidha alitoa rai kwa benki hiyo kuingia kwenye mazao mengine ili kufungua fursa zaidi kwa wakulima wa mazao mengine. “Ni fursa kubwa sana kwa mkulima mmoja mmoja na ambao wako kwenye vyama mkoani kwetu kwa Benki ya NBC kuwa kwenye sekta ya kilimo na wakulima wanatakiwa kuichamgamki waanze kuzalisha kibiashara.” Aliongeza Nd Bosco.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema kwamba Benki ya NBC kupitia NBC Shambani imejipanga vizuri kuwahudumia wateja wake kupitia matawi yake nchi nzima wakulima wa mazao mbali mbali yakiwemo tumbaku, kahawa, parachichi, pamba na chai.
Akiongelea huduma za kibenki kwa mkulima mmoja mmoja, Nd Urassa alisema kuwa mkulima anaweza kufungua akaunti bila kuwa na kianzio na kuendesha akaunti bila kuwa na makato ya kila mwezi. “Pamoja na fursa ya akaunti za shilingi na dola, akaunti za vyama vya msingi pia hazina makato lakini pia zina gharama ndogo za uendeshaji kupeleka vyama vya msingi kuendesha shughuli zake kwa gharama nafuu na kuongeza ufanisi.”
Kwa upande wake mnufaika wa zawadi ya pikipiki na Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Solelansabo, Bi Mary James Merrick aliishukuru Benki ya NBC kwa zawadi hiyo na kusema kuwa itamsaidia katika kuendesha shuguli zake za chama kwa urahisi na ufanisi zaidi. Aidha alipongeza benki hiyo kwa kutoa huduma zilizo bora na mikopo yenye riba nafuu inayowawezesha wakulima kutimiza mahitaji yao ya pembejeo kwa wakati.
No comments:
Post a Comment