Na Dotto Mwaibale, Singida.
AFISA Mtendaji Kata ya Dung'unyi wilayani Ikungi mkoani Singida Yahaya Njiku na Afisa Elimu wa kata hiyo Ester Mkoma wamekagua mradi wa maji wa Kisima Kirefu uliokwisha kamilika katika Shule ya Sekondari Dadu na kuridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh.31 Milioni fedha kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI-P4R) alisema mradi huo umetekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wao kama Serikali kazi yao kubwa ni kuikagua ili kuona kama fedha zilizotolewa na Serikali zimetumika vizuri.
"Mkuu wa shule na timu yako kwa kweli tunawapongeza kwa kuutendea haki mradi huu ambao Serikali imetumia fedha nyingi kuutekeleza " alisema Njiku.
Njiku alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kuwaomba walimu wa shule hiyo kuwahamasisha wanafnzi wao kuutunza kutokana na umuhimu wake.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi ni wajibu na wao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Mkuu wa shule hiyo Kassim Gawaza alisema fedha za mradi huo walizipokea Septemba 16 mwaka jana na zilitumika kuchimba kisima kirefu, kujenga mnara wa tenki, kuchimba na kutandaza mifumo ya maji na kujenga vinawia mikono na kuwa hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na maji salama yanapatikana na yanatumika.
Alisema kutokana na mfumo shirikishi walioutumia kutekeleza mradi huo Sh.2.4 Milioni zimebaki ambapo uongozi wa shule utajadili kuzitumia kwa shughuli zingine za maendeleo.
Uongozi wa shule hiyo na jamii kwa ujumla wanaishukuru Serikali na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa usimamizi mzuri hadi kukamilika kwa mradi huo.
Afisa Elimu wa Kata hiyo, Ester Mkoma aliwaomba wanafunzi wa shule hiyo kuutunza mradi huo na akawasihi kuzingatia masomo wakati wote wakiwa nyumbani na shuleni na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment