Na Mwandishi Wetu | Arusha | Wakristo kote ulimwenguni wametakiwa kujiandaa na kutambua kuwa kila jambo jipya linalotokea katika maisha ya Mtu linakuwa na vita vipya.
Wito huo umetolewa na Askofu Joseph Lai Laizer wakati akihubiri neno la Mungu lililokuwa na kichwa cha somo kisemacho “Jambo Jipya na Vita vipya” katika Kanisa la Christian Life Church Sinai Mlima wa Washindi lililopo Kiranyi Mkoani Arusha.
Askofu Laizer amesema kuwa kila jambo jipya linalotokea katika maisha ya Wakristo lazima yawe na vita vipya hivyo Wakristo wanapaswa kujiandaa kupambana na vita hivyo kwa silaha ya maombi pamoja na kumtolea Mungu sadaka.
“Lazima uombe maombi ya vita huku ukiambatanisha na sadaka, sadaka ni kitu cha muhimu sana”
“Jambo jengine katika kuvishinda vita hivi, yakupasa kumpata Kuhani atakayesema na kutoa matamshi juu ya hivyo vita vyako”
"Wakati Mfalme wa Israel alipoingia vitani na vita kuwa vikali alilikumbuka hili umuhimu wa kuwa na Kuhani katika vita vyako vipya ......Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hapana hapa nabii wa Bwana, ili tumwulize Bwana kwa yeye? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya..... 2Wafalme 3:11"
“Napenda kuwaasa watu wa Mungu, kuwa usifurahi sana kuwa kuna jambo jipya linakwenda kutokea kwasababu Unabii umetoka, au kwasababu Mungu amesema kupitia watumishi wake yakupasa kujiandaa na vita vipya”
“Hata mwaka kuna mambo Mungu anakwenda kufanya kwako lakini lazima ujiandae kwasababu kila jambo jipya lina vita yake” alisema Askofu.
Laiton Deo Shinze mmoja wa Waumini wa Kanisa hilo waliohudhuria Ibada hiyo alitoa maoni yake kuhusu somo hili na kusema “Kwa kweli neno la Mungu alilotufundisha leo Askofu Lai, limetufundisha kwakila jambo yatupasa tumtegemee Mungu”
Nae Bi Flomena Fredrick aliongeza kuhusu neno alilofundisha Askofu Lai “Neno la leo limenibariki sana. Mtumishi wa Mungu alikuwa anatufundisha jinsi ya kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine, yakwamba kila unapotoka hatua moja kwenda nyingine unajenga kitu kipya na kila kitu kipya huja na changamoto mpya, hivyo kuelekea hatua nyingine hupaswi kulegea, unahitajika kupambana ili kuyafikia yale mafanikio yaliyokusudiwa”
Ibada hiyo iliitimishwa kwa maombi maalumu kwaajili ya Wakristo wote Ulimwenguni. Kanisa la ‘Christian Life Church’ Sinai Mlima wa Washindi ni huduma inayopatikana katika jiji la vArusha maeneo ya Kiranyi, Sakina. Engi wanapokea na kushuhudia ukuu wa Mungu kupitia Mtumishi wake Askofu Joseph Lai Laizer.
No comments:
Post a Comment