Wadau wa elimu ya juu wamepongeza mpango mpya wa serikali kuvitaka vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu nchini kuanzisha kampasi.
Wakiongea wakati wa mahojiano na mwandishi huyu walisema mpango huu utawezesha upatikanaji wa wahitimu wenye ujuzi na wanaohimili ushindani wa soko la ajira unaokuwa kwa kasi.
“Tunaipongeza serikali kwa kuwa na mpango wa kupanua wigo wa elimu ya ufundi kwa kuvitaka vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kufundisha kozi zinazotoa ujuzi kwa wahitimu ili waweze kustahimili ushindani wa soko la ajira,” alisema Bi Angela Mungai—katika mahojiano yanayohusu masuala ya elimu ya juu Tanzania.
Maoni haya ya wadau yanakuja kufuatia tamko la Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliyoitoa bungeni hivi karibun, akihamasisha vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kuanzisha kampasi za elimu ya ufundi --kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha utoaji wa elimu inayowapa wahitimu uwezo wa ushindani watakao utumia katika soko la ajira nchini.
Akihitimisha hotuba ya makadirio ya wizara yake, Profesa Mkenda aliliambia Bunge kuwa, serikali imeweka mpango mkakati kuhamasisha vyuo vikuu kujenga kampasi za elimu ya ufundi katika mikoa mbalimbali nchini.
Pamoja na mambo mengine, Profesa Mkenda alisema mpango huu unakusudia kukuza utoaji wa elimu ya ufundi katika vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kwa kuwajengea wahitimu uwezo kwa kuwapa ujuzi unaotakiwa kwenye soko la ajira la dunia ya leo.
Waziri alikuwa akijibu maswali ya muda mrefu ya wabunge na wadau wa elimu ya juu, ambao kwa nyakati mbalimbali wamekuwa wakionyesha haja ya kuwepo kwa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kutoa wahitimu wenye ujuzi unaotakiwa kwenye soko la ajira lenye ushindani mkubwa.
“Soko la ajira linahitaji wahitimu wenye ujuzi wa kazi na siyo tu kuwa na shahada zinazoonyesha ufaulu mzuri. Tunafurahi kuona kwamba serikali imedhamiria kupanua wigo wa elimu ya ufundi hadi vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu,” alisema Bw Mohamed Unju, mbobezi katika elimu ya juu Dodoma.
Hata hivyo wadau wamesema mpango huo mpya wa Serikali hautazaa matunda kama Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU) hatarekebisha miongozo yake, wakitaja kifungu 1.5 cha Mwongozo wa Elimu ya Juu Tanzania (Toleo la 3) la Mwaka 2019, kama ni kikwazo kikachowazuia vyuo vikuu kuenga kampasi za Elimu ya Ufundi—kama inavyoekezwa katika Mpango mpya uliotangazwa na Waziri mwenye dhamana bungeni.
“Wakati umefika sasa kwa TCU kupitia mwongozo huu na kuviruhusu vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kutoa kozi zinazowapa wahitimu ujuzi unaoendana na soko shindani la ajira la dunia ya leo, mpango mpya wa serikali, ukuaji wa uchumi na mikakati ya maendeleo,” alisema bingwa wa elimu ya juu, Bw Joseph Mfutakamba.
Alipotafutwa, Msemaji wa TCU, Bi. Jorlin Kagaruki, .alisema “Sisi TCU kama wasimamizi wa Vyuo Vikuuu hatuna tatizo lolote na mpango mpya wa Serikali unaolenga kuhamasisha Vyuo Vikuu (vya Serikali na Binafsi) kujenga au kuanzisha matawi/campus yatakayotoa Elimu ya Ufundi (Technical Education Campuses)…lawa miongozo yetu (TCU haitazuia vyuo vikuu vinavyojenga au vinavyotaka kujenga matawi ya Elimu ya Ufundi, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali iliyotangazwa na Waziri Adolf Mkenda Bungeni.”
“TCU hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa Mpango wa Serikali uliotangazwa na Waziri,” amesema.
No comments:
Post a Comment