Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bi. Halima Dendego (wa tatu kulia), akionesha baadhi ya zawadi zinazotolewa kwa washindi kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” inayoratibiwa na Benki ya NBC. Wengine pichani ni Mkuu wa Kanda ya Kati wa NBC, Bw. Miraji Msuya (wa tatu kushoto), Mkuu wa Idara ya Bima wa NBC, Bw. Benjamini Nkaka (wa pili kushoto) Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa NBC, Bw. Raymond Urassa (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mkoa wa Singida (SIFACU) Bw. Julius Kitundu (kulia) na Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Singida Bi. Nuria Gulamali (wa pili kulia).
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bi. Halima Dendego (katikati), akipokea zawadi maalum ya picha yake kutoka kwa wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Kanda ya Kati wa NBC, Bw. Miraji Msuya (kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” inayoratibiwa na Benki ya NBC.
Singida, Aprili 30, 2026 — Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bi. Halima Dendego, amepongeza mchango wa wadau mbalimbali, hususan Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo. Ameitaja kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” kuwa kichocheo muhimu cha ustawi wa wakulima na ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo uliofanyika jana mkoani Singida, Bi. Dendego alisema kuanzishwa kwa mpango huo kwa mara ya kwanza katika mkoa huo ni hatua muhimu inayosaidia kufanikisha malengo ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati pamoja na kuinua kipato cha wakulima.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wakiwemo viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika, wakulima, pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Uongozi wa NBC uliwakilishwa na Mkuu wa Idara ya Bima, Bw. Benjamini Nkaka, na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima, Bw. Raymond Urassa, wakishirikiana na timu ya maofisa wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kanda ya Kati, Bw. Miraji Msuya.
Kwa mujibu wa Bi. Dendego, kampeni hiyo inaendana na mafanikio ya jitihada za Serikali ambazo tayari zimeanza kuzaa matunda. Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na usajili wa zaidi ya asilimia 92 ya wakulima mkoani Singida, utoaji wa ruzuku za pembejeo kama mbegu na mbolea, pamoja na uwekezaji katika huduma za ugani na kilimo cha umwagiliaji.
“Kampeni ya NBC Shambani inakuja kuimarisha juhudi hizi kwa kuchochea ujumuishaji wa kifedha kwa wakulima. Hii ni hatua muhimu kuelekea kilimo chenye tija na chenye manufaa kwa wananchi mmoja mmoja, kaya na mkoa kwa ujumla,” alisisitiza Bi. Dendego.
Aidha, aliwahimiza wakulima kuchangamkia fursa zinazotolewa na kampeni hiyo, ikiwemo akaunti zisizo na makato ya kila mwezi, upatikanaji wa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo, elimu ya fedha, pamoja na huduma za bima ya afya na mazao.
Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Bw. Nkaka alisema NBC inaendelea kubuni suluhisho za kifedha bunifu ili kuunga mkono azma ya Serikali ya kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030. Aliongeza kuwa benki hiyo pia inawekeza katika utoaji wa elimu ya fedha, huduma za kidijitali, pamoja na bima zinazolenga kupunguza hatari kwa wakulima.
Kwa upande wake, Bw. Urassa alisema kampeni hiyo ya miezi minne inalenga wakulima wa mazao ya dengu, choroko, mbaazi, soya na ufuta. Alieleza kuwa wakulima wana nafasi ya kushiriki binafsi au kupitia vyama vya ushirika na kushinda zawadi mbalimbali, zikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato (laptops).
“Lengo kuu ni kuwahamasisha wakulima kutumia mifumo rasmi ya kifedha kwa kutunza fedha zao benki. Tunawakaribisha kufungua akaunti za NBC Shambani ili waweze kunufaika na huduma na fursa hizi,” alibainisha.
Baadhi ya wakulima walioshiriki katika hafla hiyo walieleza matumaini yao juu ya kampeni hiyo, wakiwahimiza wenzao kuitumia kikamilifu ili kunufaika na huduma za kifedha, elimu, bima pamoja na zawadi zinazotolewa.
Uzinduzi wa kampeni ya Wekeza NBC Shambani Ushinde unaashiria hatua mpya katika juhudi za kukuza sekta ya kilimo mkoani Singida. Kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, wakulima wanapata fursa ya kuimarisha uzalishaji wao, kuongeza kipato na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.





.jpg)








